CHINA NA TANZANIA KUSHIRIKIANA KATIKA HUDUMA ZA MAKUBUMBUSHO

Makumbusho

    Makumbusho ya Taifa ya China na Tanzania zimekubaliana kushirikiana katika kubadilishana uzoefu, teknolojia na kuwa na maonesho ya pamoja kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za makumbusho zinakuwa na faida kwa pande zote mbili za nchi hizo.

    Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la China, Gazo Zheng yaliyofanyika kwenye Makumbusho ya China jijini Beijing Mei 14,2024.

    Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kwa kuwa Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu wa miaka mingi, ni vyema ikashirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika dijitali ,kufanya tafiti, kuwa na Maonesho ya pamoja, kuonesha utamaduni na historia ya nchi zote mbili pamoja na kubadilishana uzoefu wa utaalamu katika kutunza na kuhifadhi mikusanyo.

    Aidha, Mhe. Kairuki amesema kuwa Tanzania ingependa kujifunza namna ya kuvutia kizazi cha vijana kinachokua ili kiwe na utamaduni wa kutembelea Makumbusho mbalimbali zilizopo nchini Tanzania.

     Amesema Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake ulipo jijini Beijing nchini China utahakikisha unafuata taratibu zote za kuwepo kwa Mkataba wa Makubaliano kati ya makumbusho hizo ili kurasimisha ushirikiano huo.

     Kwa upande wake, Mkurugenzi Zheng amesema Makumbusho ya Taifa la China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote yaliyopendekezwa.

    “Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu mkubwa na ina wataalamu zaidi ya 2000 hivyo ina furaha kushirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania hasa katika kuhifadhi mikusanyo, kufanya tafiti, kubadilishana uzoefu na namna ya kuvutia vijana kuwa na utamaduni wa kutembelea makumbusho” amesema.

    Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma.

 

stories
standard
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.