Hali ya Uchumi wa Zanzibar inakadiriwa kukuwa kwa Mwaka 2024 kwa wastani wa Asilimia 7 nukta 2 kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ongezeko la uingiaji watalii wanaoitembelea Zanzibar kwa Asilimia 30 pamoja na utekelezaji wa Miradi mikubwa ya kimkakati
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ,Fedha na Mipango Dkt.Saada Mkuya Salum amezitaja sababu nyengine kuwa ni kuongezeka uhamasishaji wa ukusanyaji Mapato na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza thamani
Amesema misingi mikuu ya kukidhi ufikiaji wa matarajio hayo ni kuimarika kwa usimamizi wa Sera za Kifedha pamoja na kuimarika upatikanaji wa Nishati ya mafuta na gesi ili kupunguza gharama za Bei ya nishati hizo
Akizungumzia kuhusiana na vipaumbele vya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 amesema ni Serikali kuchukuwa hatua za kisera katika kuimarisha Mapato na kusimamia Matumizi ya Serikali kwa kuimarisha usimamizi wa Kodi pamoja na kuimarisha uwajibikaji wa Wakuu wa Taasisi zinazojitegemea ikiwemo Mashirika na Mamlaka
Aidha amesema kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Kiwango cha utegemezi wa Bajeti ya Serikali kinakadiriwa kufikia Asilimia 6.3 kulingana na matarajio ya kupokea Bilioni 322 Nukta 9-5 ikiwa ni misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo
Kuhusiana na mazingatio ya Maeneo mahsusi kwa Bajeti ya 2024/2025 Dkt.Saada amefahamisha kuwa ni pamoja na kuanza Malipo ya Nauli, kwa Watumishi wote wa Serikali kwa kutenga Bilioni 34 ,na kuongezeka kwa Posho la Likizo kwa Watumishi hao kwa kutenga zaidi ya Shilingi Bilioni 2
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameombwa kuidhinisha zaidi ya Shilingi Trilioni 5.1 kwa ajili ya Matumizi ya Serikali kwa kazi mbali mbali ikiwemo kazi za kawaida na Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2024/2025