Wadau wa Vyombo vya Habari Nchini wameibua tena kilio chao cha kupatikana kwa sheria ya habari hapa Zanzibar na kwa kauli moja wameitaka Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo kuhakikisha wanaikata kiu yao ya muda mrefu ya kuipata sheria hii.
Huu ulikuwa ni Mkutano mahususi kati ya Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo na Wadau wa Sekta ya Habari ukiwa na lengo la kupata maoni, ushauri kero na mjadala wa kujenga uhuasiano mwema kati ya Sekta ya Habari na Wadau wake.
Huu ulikuwa ukurasa mpaya wa uhusiano kati ya Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo na Wadau wa Sekta ya Habari Nchini.
Jopo la Uongozi la Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo ukiongozwa na Waziri wake Dkt. Riziki Pembe Juma, ukakaa kimya hapa kuyasikia ya Wana habari.
Kilio cha Takribani Miaka 20 cha upatikanaji wa Sheria ya Habari kikasikika kutoka kwa Wanahabari.
maslahi ya Wana habari nayo yakatajwa hapa. licha ya kazi nguvu ya kuuhabarisha Umma, lakini maslahi ni kiduchu mno.
Baadhi ya Wamiliki wa Vyombo vya Habari wakalalamikia milolongo ya Kodi jambo wanalodai linawaumiza kwa kuwa hakuna Mapato yanayoendana na Kodi wanazotozwa.
Kikao hiki kilikuwa na tamu na chungu zake. baadhi ya Vyombo vya Habari vikakumbushwa kuhusu matumizi sahihi ya lugha adhimu ya Kiswahili na wengine wakisifia uthubutu wa kutoa Habari zinazoigusa Jamii na uwajibikaji wa Serikali.
Hoja hizi za Wadau wa Habari zikapata ufafanuzi mdogo wakati majibu kamili yakiandaliwa.
Matar Zahor Masoud, ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, anasema Mkutano huu umeipa Wizara sababu ya kuchora upya Ramani ya namna kuendesha shughuli za Wizara.
Naibu Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Ali Abdulgulam Hussein anasema Mkutano huu unatekeleza maagizo ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi na hivyo ametoa rai ya kutaka ushirikiano na Wadau wa Sekta ya Habari ili kufanikisha malengo mazuri ya Serikali.
Mwisho akafunga Mwenyekiti wa Mkutano huu Dkt. Rikizi Pembe Juma, Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo na kwanza anawakumbusha Wadau wa Habari hatua zinazopaswa kufuatwa ili kuipata sheria ya Vyombo vya Habari.
Ushauri wa Dwisho wa dkt. Riziki Pembe Juma ni kwa Wadau wa Sekta ya Habari kuukuza umoja wa Wana-habari ili kurahisisha usikilizwaji wa malalamiko yao na kuyapatia ufumbuzi.





