Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya sekta ya elimu ili kuwawezesha vijana kusoma fani tofauti ndani ya Nchi.
Rais wa Zanzibar ameyasema hayo katika mahafali ya 19 ya Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA na kuwatunuku vyeti, stashahada, shahada, shahada za uzamili na uzamivu kwa wahitimu wa Chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2022/2023, huko Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Dkt Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji watu wenye uwezo wa kujifunza kwa haraka, wenye kujituma wenye kufikiri namna ya kutatua matatizo ya jamii, inayowazunguka na waliyotayari kujitolea kwa maslahi ya Nchi huku akisema Serikali inajivunia mafanikio ya Chuo hicho hasa katika ongezeko la Wahitimu kila mwaka.
Aidha amesema Serikali za Tanzania zimejiandaa kuhakikisha Vijana wote wanaotaka kujiendeleza wanapata mikopo ya elimu juu pamoja na kuhakikisha inatatua matatizo ya uhaba wa Wataalamu na Majengo.
Aidha Dkt Mwinyi amemtunuku shahada ya uzamivu ya heshima katika sekta ya Utalii na Masoko Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika sekta hiyo na kusema kuwa dhamira yake inalengo la kuwaletea maendeleo Wananchi na kuimarisha ustawi wao.
Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Lela Mohamed Mussa amesema sekta ya elimu imekuwa ikiimarika kutokana na juhudi za Serikali za kuweka mazingira mazuri ya elimu.
Makamu mkuu wa SUZA, Prf. Mohammed Makame Haji amesema Chuo kinaimarika na idadi ya wanaojiunga na Chuo inaongezeka siku hadi siku.
Katika Mahafali hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunikiwa shahada ya heshima ya uzamivu ya usimamizi wa Utalii na Masoko ya Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA.