Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Lindi limeendesha oparesheni maalumu ya kudhibiti vitendo vya kujiunganishia umeme kiholela na kinyume cha sheria, ambapo limefanikiwa kuwakamata watu wawili wanaodaiwa kujiunganishia huduma hiyo bila kufuata taratibu.
Watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Hassan Gayo Mkonde pamoja na Mr. Thomas, wanaotuhumiwa kuunganisha umeme kinyume cha sheria. Oparesheni hiyo imefanyika katika kijiji cha Pangatena, Kata ya Nachunyu, Halmashauri ya Mtama, Wilaya ya Lindi, ambapo TANESCO imebaini kuwa mwekezaji wa kisima cha maji kijijini hapo alikuwa amejiunganishia umeme kinyume na utaratibu, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Lindi, Theodory Holl, amesema oparesheni hiyo ilifanyika baada ya shirika kupokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu uwepo wa mteja aliyejiunganishia umeme kwa njia ya kificho, jambo linalohatarisha usalama wa watumiaji na miundombinu ya umeme.

Aidha, Holl amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na TANESCO kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vya matumizi au uunganishaji wa umeme unaotia shaka. Kwa upande wao, Wenyeviti wa Kitongoji cha Pangaboi na Kijiji cha Nachunyu wamesema kuwa mradi wa maji uliopo kijijini hapo umekuwepo na kutumika kwa muda mrefu, hata hivyo hawakuwa na ufahamu kuwa mwekezaji wa mradi huo alikuwa amekiuka sheria na taratibu za uwekaji wa umeme. Wameeleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa wananchi, hususan kwa kuwa unatumika pia katika Kituo cha Afya cha Pangaboi. Naye Mtendaji wa Kijiji cha Nachunyu, Hassan Mohammed, amesema kuwa serikali ya kijiji inaufahamu mradi wa maji wa Pangaboi, lakini hakujua kuwa mwekezaji wake alikuwa ameunganisha umeme kinyume cha sheria.
