Basi la Kampuni ya Kisire limegongana uso kwa uso na lori katika eneo la mnada wa Tinde Wilaya ya Shinyanga na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine 12 wakijeruhiwa na kukimbizwa Kituo cha afya Tinde kupata matibabu.
Ajali hiyo imehusisha basi la Kisire lenye namba za usajili T 229 EEL, lililokuwa likitoka Kahama kuelekea Mwanza, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lenye namba za usajili RAE 849N. lililokuwa limebeba shehena ya mchele kutoka Dar es Salaam kwenda nchi jirani ya Rwanda huku chanzo kikielezwa kuwa ni mwendo kasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi amesema aliyefariki ni dereva wa lori hilo, huku majeruhi 12 wanaendelea kupatiwa matibabu huku watano wanahali hali mbaya wanaendelea kupatiwa huduma za dharura chini ya uangalizi wa madaktari bingwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na saba wanapatiwa matibabu Kituo cha afya Tinde.

Kamanda Magomi amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe na mwendokasi, unaodaiwa kufanywa na dereva wa lori ambaye alitaka kulivuka gari lililokuwa mbele yake akijaribu kulivuka gari lililokuwa mbele na kukwepa mkokoteni uliokuwa umebeba matikiti maji yaliyokuwa yanapelekwa mnadani.
