BALOZI SAID OTHMAN AWATAKA WATANZANIA WAISHIO NCHINI COMORO KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA

Balozi Comoro

     Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro amekutana na Watanzania wanaoishi nchini Comoro na kuwaasa wawe mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuitangaza vyema Tanzania katika jumuiya za kimataifa.

     Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa Watanzania na kueleza mikakati yake pamoja na Ubalozi katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro.

     Alifahamisha kuwa wananchi wa Comoro wana mapenzi na mahusiano ya karibu na Tanzania. Familia nyingi nchini humo zina ndugu zao upande wa Tanzania. Hivyo, Nchi mbili hizi zina wajibu wa msingi kuimarisha ushirikiano ili kulinda na kuendeleza tunu hiyo muhimu.

    Aidha, Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu alifahamisha kuwa Ubalozi una wajibu wa msingi kushughulikia maslahi ya Watanzania nchini humo. Alifahamisha kuwa kwa upande wake aliwasihi Watanzania kuunga mikono juhudi za maendeleo nchini Tanzania kwa kuwa Mabalozi wazuri wa Nchi yao, kutangaza fursa zinazopatikana nchini na kuwaunganisha Watanzania na Wakomoro ili watumie manufaa ya ushirikiano wa kindugu na kihistoria uliopo baina ya Nchi hizi mbili.

     Nao Watanzania wanaoishi nchini Comoro walimshukuru Mhe. Balozi Saidi Yakubu kwa hekima na uamuzi wa kuwaona siku chache baada ya kuwasili nchini Comoro. Waliahidi kumpatia ushirikiano na kufuata nasaha zake na waliwasilisha changamoto kadhaa na kuomba zizingatiwe wakati wa mikutano na vikao vya mashauriano katika ngazi ya Kiserikali ili ziweze kupatiwa ufumbuzi. Miongoni mwa maeneo hayo ni changamoto ya visa, kukosekana Bima za mizigo, na ukosefu wa usafiri wa uhakika baina ya Nchi hizi mbili.

 

stories
standard
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.