Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kudumisha amani, mshikamano na upendo na kamwe wasigawanywe kwa sababu yoyote.
Amesema hayo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Robert Yondam Pangani wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi iliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji mkoani Mbeya.
“Nimefurahi kusikia wewe ni mtu mtulivu na myenyenyekevu sana upokee jambo hili kwa amani, nina imani eneo lako la mahubiri litakuwa kubwa zaidi na sisi tutaendelea kukuombea kwa Mungu ili lile aliloweka ndani yako liweze kujitokeza”, amesema Dkt. Biteko.
Ametoa wito “Waumini wenzangu huyu si malaika ni binadamu itafika wakati atachoka naomba mumtie moyo, na msiache kumuombea na kumtii inawezekana kuna anayejua kuliko yeye lakini yeye amepewa fursa ya kuwaongoza nyinyi hivyo mumtii. Pia tusibaguane kwa dini zetu au vyama vyetu vya siasa, sisi tuliokaa hapa hatujatambuana kwa makabila yetu tunatambuana kwa utanzania wetu, wakati wote muhubiri amani na mtu yeyote mwenye shida aone Tanzania ni mahali salama” .
Pia, amemsii Askofu Pangani kuwasikiliza watangulizi wake pamoja na Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania kwa kuwa wana heshima na hekima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera amesema kuwa Mhe.Rais Samia ameunganisha taasisi za dini na alichangia milioni 50 katika Kanisa la Moravian kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mkoani Dodoma.
“ Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati naomba utusaidie katika mgogoro wa kiwanja mkoani Dodoma ili waweze kujenga ofisi zao, Rais Samia yuko pamoja nao na ameunganisha taasisi za dini na ukiona taasisi hizi ziko pamoja ni jitihada zake hasa hapa Mbeya”, amesema Mhe. Homera.