Akifungua Skuli ya Sekondari ya Wanawake ya Ghorofa Tatu ya Utaani iliyojengwa baada kuungua moto Mwezi Machi Mwaka 2022 amesema, Ujenzi wa Skuli hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa baada ya tukio la moto lililoteketeza Skuli ya Awali iliyokuwa na Madarasa 11.
Hivyo ameiagiza Wizara ya Elimu kusimamia Ujenzi uliobaki wa Ukumbi wa Mikutano na Uwanja wa Michezo itakayoendana na hadhi ya mwonekano mzuri wa Skuli hiyo na kuahidi kujenga Dakhalia kubwa ya kisasa.
Wakati huo huo Dkt.Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kujenga Bandari ya kisasa Wete ambapo hatua za awali za ujenzi huo zimekamilika pamoja na kuzifanyia matengenezo makubwa Nyumba za maendeleo na kujenga nyumba mpya Unguja na Pemba.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe.Lela Mohammed Mussa ameahidi kuwa Wizara itaendeleza juhudi za Serikali kwa kuzitunza Skuli zote ili kubaki kwenye ubora wake.
Mwakilishi wa Jimbo la Wete, ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Harusi Said Suleiman amemshukuru Rais Mwinyi kwa kuendelea kuimarisha maendeleo Nchini ikiwemo Barabara safi za Mijini na Vijini, Ujenzi wa Skuli za Ghorifa pamoja na huduma za Jamii za afya na maji safi na salama.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe.Salama Mbarouk Khatib amesema Wananchi wa Mkoa huo wanaendelea kuimarisha umoja na mshikamano ili kuimarika kwa maendeleo yao na ya Nchi.
Akitoa Salamu za Chama cha Mapinduzi, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM - Taifa, Omar Kilupi amesema Ufunguzi wa Skuli hiyo ni utekelezaji wa ilani ya Chama hicho ya 2020 – 2025 ambayo tayari imepitiliza malengo iliyojipangia kuwaletea Wananchi Maendeleo.
Ujenzi wa Skuli ya Sekondari Utaani ulioanza Mwezi Mei Mwaka Jana umegharimu Shilingi Bilioni 6 Nukta 2 ikiwa na Madarasa 41, Maktaba, Maabara, Chumba cha Kompyuta na Ofisi ya walimu.