Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza taarifa maalum ya udhibiti wa vitendo vya uvuvi haramu iwasilishwe kabla ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya Bajeti ya Mwaka 2024/2025.
Ametoa agizo hilo (Jumapili, Aprili 21, 2024) katika hafla ya uzinduzi wa boti maalum kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari hapa nchini iliyofanyika bandarini jijini Dar es Salaam.
“Taarifa kuhusiana na shughuli maalum ya udhibiti wa vitendo vya uvuvi haramu katika ukanda wa Bahari kuu iwasilishwe kabla ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025,” amesema.
Ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha mipango ya maendeleo ambayo imechangia dola za Marekani 500,000 kwenye ununuzi wa boti hiyo. “Ninaiomba Serikali ya Japan isichoke kutusaidia ili tuweze kukamilisha utekelezaji wa mikakati iliyopo katika eneo hili la kukabiliana na uhalifu nchini,” amesema.
Vilevile, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuchangia dola za Marekani 400,000 kwenye mradi huo. “Mchango wenu tunauthamini sana, wakati wote mmekuwa mkishirikiana nasi katika maeneo mengi, kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Tanzania ninawashukuru sana,” amesema.
Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga alieleza kuwa ununuzi wa boti hiyo ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu unaotekelezwa na Serikali.
Akieleza sifa za boti hiyo alisema: “Ni boti ni mpya, ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuhimili utekelezaji wa majukumu ya doria. Boti hii ya doria imepewa jina la Patrol Boat Sailfish (PB Sailfish)