Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar kimewashauri Wahariri wa Vyombo vya Habari kuzipitia kazi zinazowasilishwa katika Tunzo za Takwimu za Wanawake na Uongozi ili ziweze kuwa na ubora.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Majumuisho ya Hafla ya utoaji tunzo zilizotolewa hivi karibuni, Mkurugenzi wa TAMWA, Zanzibar, Dkt.Mzuri Issa, amesema baadhi Waandishi wa Magazeti na Redio, waliowasilisha kazi zao, hazikuwa na kiwango cha kuridhisha kutokana na kutopitiwa na Wahariri.
Amesema kwa upande wa Makala za Televisheni, hakuna mshindi aliepatikana kutokana na kazi zao kutokuwa na Vigezo, hivyo amewataka Wahariri kuhakikisha wanashirikiana na Waandishi wao ili waweze kupata ushindi unaokubalika.
Akiwasilisha Tathmini walioifanya baada ya kupitia kazi hizo Kiongozi wa Majaji wa Tunzo hizo Dkt.Abdalla Muhammad Juma, amesema mashindano hayo yanawaimarisha Waandishi chipukizi kuibua Habari na matukio mbali mbali katika Jamii.
Amesema zaidi ya kazi mia tano za Waandishi wa Habari zimewasilishwa kwao ili kumtafuta Mshindi ambapo Wanawake wengi wamejitokeza na kushinda nafasi mbali mbali za Tunzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari za Kijamii.