Jumla ya Shilingi Bilioni 1 Nukta 5 zinatarajiwa kutumika katika Kampeni maalum ya afya bora Maisha bora kwa kuwapima na kupata Matibabu bure Wananchi wenye Magonjwa mbalimbali kwa Zanzibar.
Akizungumza katika Viwanja vya Hospitali ya Kivunge wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Siku 5, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Rashid Hadid Rashid amesema Serikali inatumia gharama kubwa kuwapeleka Wagonjwa Nje kupata Tiba hivyo Kampeni na Kambi hizo zitapunguza hali hiyo kwa kiasi kikubwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha bora Foundation (ZMBF) Fatma Fungo amesema wanategemea kufikia Watu Elfu 5 kwa Siku Tano za Kambi hiyo iliyoanza Machi 4 hadi 8 na kuhitimishwa kwa matembezi yatakayoongozwa na Mwenyekiti wa (ZMBF) mama Mariam Mwinyi.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya wa Wizara ya Afya Dk Salim Slim amesema kupitia Kambi ya awali, wamegundua Watu wengi wakiwa na Magonjwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi lakini hawajitambui na kuambukiza wengine.
Kampeni hiyo inayohusisha huduma za upasuaji, uchunguzi wa Tezi Dume, Macho, Moyo na Masuala ya Uzazi inaendeshwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya (ZMBF) ikitarajiwa kuwafikia Wananchi Elfu 20 katika Mikoa yote ya Zanzibar kwa kipindi cha Miaka Mitatu.