Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ameshiriki kisomo cha Dua khitma alichokiandaa kwa ajili ya Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili Tanzania.
Kisomo hicho kilichofanyika katika Viwanja vya Maonesho Nyamazi kimehudhuriwa na Viongozi na Wananchi mbalimbali.
Akitoa Wasifu wa Marehemu Mzee Mwinyi Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi amesema alikuwa Kiongozi wa Nchi mbili Zanzibar na Tanzania na amefanya uadilifu na kuzifungua Nchi hizo kiuchumi na kuleta neema kubwa kwa Watu wa Nchi Jirani ikiwemo Kenya na Somalia.
Amesema Marehemu alikuwa akijishusha kwa Watu, akiwatukuza Maulamaa na Kuwaheshimu Masheikhe mbalimbali na kuwaenzi hali hiyo imetokana na unyenyekevu hivyo amehimiza Watu kuwa wanyenyekevu na kufanya heri katika kumcha Allah.
Akitoa Shukran katika Kisomo hicho Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Hussein Mwinyi amewashukuru wote waliokuwa wakimuombea Dua wakati wa ugonjwa wake na kushiriki katika kumzika Marehemu Baba yake .
Akitoa Nasaha katika kisomo hicho Sheikh Othman Maalim amesema Marehemu Mzee Mwinyi ni Kiongozi Mwenye hekima na busara kubwa hali iliyosababisha Nchi nzima kuwa katika majonzi na huzuni kubwa.
Dua hiyo imehudhuriwa na Viongozi wa Umma na Binafsi pamoja na Wananchi mbali mbali.