Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Philip Mpango amesema makusanyo ya Kodi Nchini Tanzania yamekua chini ya Asilimia 12 ya pato la Taifa kwa Takriban muongo mmoja sasa kiwango ambacho ni chini ya wastani wa asilimia 15.6 kwa Nchi za Bara la Afrika.
Akizindua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 kwa niaba ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan, Dr. Philip Mpango amesema Serikali inatoza kodi na kutafuta Mikopo na misaada kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa Serikali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo wawekezaji na Wafanyabiashara wasipolipa kodi ipasavyo hudhoofisha uwezo wa Serikali kutimiza wajibu wake.
Amesema kuwa kumekuwa na mtazamo uliojengeka kuwa mfumo wa kodi ni kikwazo katika ufanyaji wa Biashara na uwekezaji hali inayothibishwa na malalamiko ya waekezaji ambayo ameyataja huku akiainisha maboresho yaliyofanywa na Serikali ili kuondosha malalamiko hayo.
Amesisitiza juu ya umuhimu wa wawekezaji na Wafanya biashara kulipa kodi na kuwataka Mawaziri wa Sekta kuzingatia maoni yatakayotolewa naWashiriki wa Jukwaa hilo na kuwasihi Washiriki kutoa michango itakayoibua njia za kuongeza mapato ya Serikali bila ya kuwaumiza Wafanya biashara na wawekezaji.
Akimkaribisha Makamu wa Raisi Waziri wa Fedha Dr. Mwigulu Nchemba amesema Taifa bado linakabiliwa na changamoto ya matumizi ya Mashine za efd’s na kuanisha mbinu mbalimbali zinazotumiwa na Wafanyabiashara katika kukwepa ulipaji wa Kodi.
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi (Mipango na Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo amesema kwa sasa Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kupokea Wawekezaji kutokana na maboresho ya Sheria, Sera, na kanuni yaliyofanyika yakilenga kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.
Dr .Juma Maliki ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar amesema ushirikiano kati ya Vituo vya uwekezaji vya TIC na ZIPA umesaidia kutatua changamoto za kikodi huku Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafisi Raphael Maganda akiishauri TRA namna bora ya kuongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi.
Kongamano la Kodi na Uwekezaji ni la Siku Mbili na linalenga kukusanya maoni ya Wadau ambayo yatatumika katika mchakato wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha unaofuata.