Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imekabidhi gawio la Sh 7 Bilioni kwa mwanahisa wake wa pekee Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kufuatia faida iliyopata katika kipindi cha mwaka 2023. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inamiliki asilimia 100 ya hisa za benki hiyo.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ, Bw Arafat Haji alikabidhi gawio hilo kwa Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango – Zanzibar Dkt. Saada Mkuya Salum aliewakilisha serikali ya SMZ wakati hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika jana kwenye Ukumbi wa Mikutano, Makao Makuu ya PBZ, Mpirani, Zanzibar huku ikienda sambamba na Mkutano wa Mwaka wa Wanahisa (AGM).
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Dkt Mkuya pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2023, aliwasilisha salamu za Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Ally Mwinyi ambae pia aliipongeza benki hiyo huku akitoa wito kwa taasisi na mashirika yenye umiliki wa umma kuhakikisha yanatimiza wajibu wao wa kuwasilisha gawio litokanalo na faida za uendeshaji wa shughuli zao kwa serikali.
"Serikali inafurahishwa na mafanikio mnayoendelea kuyapata na msisitizo wetu kwenu nyinyi kuedelea kujiendesha kwa ufanisi na uweledi. Sisi kama wanahisa, tunafurahi kuona uwekezaji wetu unatoa matunda. Gawio hilo la 7 bilioni ambalo Serikali imelipokea leo litaongeza ukubwa wa kapu letu la makusanyo ambayo yamekuwa yakielekezwa katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ile ya kimkakati. Hivyo naipongeza sana kwa mafanikio haya…hongereni sana,’’ alisema Dkt Mkuya.
Awali akizungumza kwenye tukio hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa BPZ Bw Joseph Meza alieleza kuwa mafanikio na mwenendo chanya wa benki hiyo unathibitisha imani kubwa waliyonayo wateja kwa kwa benki hiyo.