Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Dk. Saada Mkuya Salum amewataka Watendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (Pbz) kuipa ushirikiano Bodi mpya ili waweze kuyapeleka mbele zaidi mafanikio ya Benki hiyo.
Akizindua Bodi mpya ya Pbz Dkt.Saada amesema mafanikio yaliyopatikana ni makubwa ukilinganisha na walipotoka ambapo bado kuna fursa katika Soko hivyo anaamini ushirikiano huo utawawezesha kufika lengo la Serikali.
Dkt. Saada amefahamisha kuwa mafanikio makubwa ya Serikali yanatokana na mchango wa Benki ya Watu wa Zanzibar hivyo juhudi zaidi zinahitajika ili kupeleka mbele maendeleo ya Benki hiyo na Taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Ndg.Joseph Abdalla Meza amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kumuamini na kuahidi kuyafanyia kazi yote waliyoelekezwa kwa kufuata sheria zilizopo ili kufikia lengo la kuanzishwa kwa Benki hiyo.