Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta imeanza kufanya tathmini Nchi nzima kubainisha maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho kukabiliana na athari za Kimazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Khalifa Mohammed Issa aliyetaka kujua lini Serikali itafanya utafiti kuyabaini maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti maalumu Mhe. Mariam Nasoro Kisangi aliyeuliza mkakati ya Serikali wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, Naibu waziri ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inaendelea na kampeni za kuhamasisha Wananchi kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo zoezi la upandaji wa Miti katika maeneo yote Nchini.
Mhe. Khamis ameibainisha kuwa Serikali imeandaa na kutekeleza mkakati wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) na mpango Kabambe wa taifa wa hifadhi ya Mazingira (2022-2032).