Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekutana na Balozi mdogo wa China Mhe. Zhang Zhisheng anayefanyia kazi zake Zanzibar, kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi Nchini.
Rais Dk Mwinyi amemshukuru Balozi Zhang kwa kudumisha na kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Zanzibar na China katika miaka mitatu ya utumishi wake Nchini.
Ameleza kuwa China imeendelea kusaidia Zanzibar na kushirikiana katika Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Sekta ya Afya, ufadhili wa Masomo, Biashara, Utalii, pamoja na kuwepo kwa Kampuni za Kichina katika kazi za Miradi mbalimbali ya Miundombinu ya Barabara, Bandari, na Uwanja wa Ndege.
Aidha amewakaribisha wawekezaji kutoka China kwenye Sekta ya Utalii na kueleza kuwa Zanzibar itaendelea kushirikiana na kudumisha uhusiano na China ambayo yametimiza Miaka 60.
Balozi Mhe.Zhang Zhisheng amesema China itaendelea kushirikiana na Zanzibar kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia.