Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imesema Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani utahusisha Bandari za kisasa, Miundombinu na maeneo ya uwekezaji.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi huo mbele ya kamati ya Bajeti Waziri wa ujenzi, mawasiliano na uchukuzi Dkt. Khalid Salim Mohamed amesema ujenzi huo utajumuisha Bandari ya mizigo mchanganyiko, Bandari ya Mafuta na Gesi, eneo la kuwekea Makontena, kuhifadhia Mizigo, Barabara, Viwanda, Makaazi, Elimu, michezo na maeneo mengine.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa za malipo ya fidia kwa Wananchi walioathirika na mradi huo Dkt Khalid amesema hatua mbali mbali zimechukuliwa ikiwemo baadhi ya Wanachi kulipwa fedha zao na ujenzi wa Nyumba zinazoendelea kujengwa kwa ajili ya Wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe Mwanaasha Khamis Juma ameishukuru Serikali kwa mtazamo wa kutoa muongozo wa ulipaji fidia kwa Wananchi wanaomiliki Ardhi.
Aidha kamati ilipata fursa ya kutembelea eneo la Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani ili kujionea namna ujenzi unavyoendelea ukiwemoujenzi wa Nyumba za fidia za Wananchi unavyoendelea.