Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla, ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa marekebisho ya Bandari ya Mkoani na maegesho ya makontena ikiwa ni mwendelezo wa shamra shamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema uendelezaji wa miundo mbinu ya Bandari kisiwani Pemba itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara pamoja na kuwanufaisha wananchi kupata nafuu ya ununuaji wa bidhaa kutokana na Bandari kuwa na uwezo wa kupokea Meli kubwa ambazo zitashusha mizigo moja kwa moja kisiwani Pemba kutoka nchi jirani.
Aidha Mhe, Hemed ameuagiza uongozi wa Shirika la Bandari kuvitunza vitendea kazi ili ziweze kutumika kwa muda mrefu, pamoja na kuhakikisha mapato yanaingia Serikalini kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuitumia Bandari hiyo kwa Abiria na wafanyabiashara huku akiwataka wananchi kuwa watulivu na kudumisha umoja na amani iliyopo.
Nae waziri wa Ujezi, Mawasiliano, na Uchukuzi Dkt. Khalid Salum Muhammed, amefahamisha kuwa Bandari ya Mkoani itazidi kutanuliwa na eneo la kina cha Maji kuongezeka kutoka mita saba (7) iliyopo sasa na kufikia mita kumi na moja (11) ili kuziwezesha meli kubwa kutoka nje ya nchi kufunga gati wakati wowote na kutoa huduma kwa wananchi wa kisiwani Pemba.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Akif Ali Khamis, amesema matengenezo yaliyofanyika katika Bandari ya Mkoani yanaendana na matakwa na viwango vya Kimataifa vya usimamizi wa Bandari ambayo yatatoa nafasi kwa meli za Kimataifa na meli za mizigo kuweza kupakia na kushusha katika Bandari hiyo.