Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amejivunia kufikia asilimia 150 ya malengo ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa Ujenzi wa Skuli mpya Unguja na Pemba hivyo kuvuka malengo ya ilani ya CCM 2020-2025 iliyoelekeza kujengwa madarasa 1,500 ya Msingi na Sekondari Unguja na Pemba kwa miaka mitano.
Amesema hayo alipoweka Jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Utaani Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini pemba katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema ni matumaini yake uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali kuimarisha Miundombinu katika Sekta ya Elimu utachochea zaidi ufaulu wa Wanafunzi.
Aidha amemtaka Mkandarasi wa ujenzi wa Skuli hiyo Benchmark na Wakala wa Majengo Zanzibar kumaliza ujenzi wa Skuli ya utaani Mwezi Machi mwaka huu.
Naye, naibu Katibu Mkuu CCM zanzibar dkt. Mohamed Said Dimwa amempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuvuka malengo ya utekelezaji wa ilani ya CCM 2020-2025 katika sekta ya elimu Nchini.
Mbunge wa jimbo la Wete kupitia chama cha ACT wazalendo Mhe Omar Ali Omar amepongeza hatua ya maendeleo yanayofanywa na Dkt. Mwinyi.
Mara baada ya hafla hiyo Dkt. Mwinyi ametembelea ghala ya Shirika La Biashara la Taifa Zanzibar ambapo alishuhudia tani 9 nukta 5 Karafuu za Magendo zilizokamatwa ambazo zina thamani ya shilingi milioni 140.