WAZIRI TABIA AWAOMBA VIONGOZI PAMOJA NA WANANCHI KUSHIRIKIANA KATIKA MAPOKEZI YA MBIO ZA MWENGE

Waziri Tabia

     Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewaomba viongozi, wafanyakazi, vikosi vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kushiriki katika mapokezi ya mbio za mwenge mwaka 2024.

      Mhe. Tabia ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na mapokezi ya mbio za mwenge wa uhuru kwa upande wa Zanzibar.

     Amesema mwenge wa uhuru mwaka 2024 kuwasili Zanzibar tarehe 13 mei 2024 na kutembezwa katika Mikoa na Wilaya zote za Unguja na Pemba.

     Amesema mbio hizo, zinaelimisha na kuhamasisha jamii ya watanzania kuhusu kuzingatia lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI dawa za kulevya na ugonjwa wa Malaria.

     Aidha amesema ujumbe wa mbio za mwenge mwaka huu unalengo la kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wote wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hususan Tanzania bara kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na utulivu.

     Sambamba na kuendelea kushiriki kikamilifu katika harakati za kuhifadhi mazingira kwa ujenzi wa Taifa.

     Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya vijana Zanzibar Shaibu Mohd Ibrahim amesema maandalizi ya mbio hizo yamekamilika na miradi mbalimbali yakiwemo ya Vijana, Afya na wajasiriamali inatarajiwa kuzinduliwa katika mbio hizo.

     Aidha amesema mwenge wa uhuru upo kwa watu wote na hauna ubaguzi wa rangi, siasa , dini wala kabila hivyo ni vyema wananchi hususan vijana kujitokeza ili kuweza kufanikisha mbio hizo.

     Mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024, zimezinduliwa rasmi tarehe 02/04/2024 katika kiwanja cha chuo cha ushirika moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo Mgenirasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

     Na ujumbe wa mwenge wa uhuru mwaka huu ni Uhifadhi wa mazingira na uchaguzi wa Serikali za Mitaa chini ya kauli mbiu isemayo tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu.

 

stories
standard
 
The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.