Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amaendelea kusisitiza ifikapo kesho Alhamisi Mei 9,2024 mawasiliano ya barabara barabara ya Lindi - Dar es Salaam yatarejea ambapo tayari eneo la somanga limeanza kupitika .
Bashungwa ameyasema hayo Mei 08, 2024 Mkoani Lindi wakati akisimamia zoezi la urejeshaji wa miundombinu ya barabara hiyo ambayo iliharibiwa mvua za El-Nino siku ya Jumamosi zilizombatana na Kimbunga Hidaya.
“Kwa namnna tulivyojipanga tuliahidi watanzania kuwa hadi kufikia Alhamisi barabara hii tutakuwa tumerudisha mawasiliano na tayari kipande cha Somanga kilichokuwa kimekatika kwa mita 200 tumeshakikamilisha na hivi sasa nguvu zote tunazielekeza katika eneo la Songas na kuendelea katika maeneo mengine”, amesema Waziri Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza changamoto zinazowakabili wataalam ambao wanaendelea kurejesha mawasiliano katika barabara hiyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa mawe ambayo yanafuatwa Kigamboni na Boko-Magereza mkoani Dar es Salaam, huku zoezi hilo likifanyika usiku na mchana.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack ameipongeza timu ya wataalamu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Makandarasi na wasaidizi wake pamoja viongozi wa Wizara ya ujenzi na uchukuzi
“Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha mawasiliano yanarejea , wakati mvua zinanyesha ile siku ya kwanza watu 31 waliokuwa katika kituo cha kuchakata gesi asilia SONGAS walishindwa kuokolewa kutokana na kuzingirwa na Maji” alisema Telack.