Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mhe.Masoud Ali Mohammed, ameitaka Kamati ya Uongozi ya Ofisi yake, kuhakikisha Miradi ya Mwaka 2023/24 iwe imekamilishwa na ianze kutumika.
Akizungumza na Kamati hiyo ya Uongozi katika Ukumbi wa Makao Makuu ya KVZ Mtoni amesema kukamilika kwa Miradi hiyo kutatoa nafasi ya utekelezaji wa Miradi mipya iliyobuniwa ambayo itawalenga Wananchi kwa kuendeleza shughuli zao kwa kujiongezea Kipato na kukuza pato la Nchi.
Aidha Waziri Masoud amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kuhakikisha kuwa vitendo vya kihalifu vinakomeshwa, ili Amani na Usalama izidi kudumu katika Maeneo yao.
Nae Mkurugenzi Mipango Sera na Utafiti, Abdullah Issa Mgongo, amesema Wizara imefanikiwa kuratibu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na Shughuli nyengine za kisekta, kwa lengo la kuhakikisha huduma zote muhimu za Serikali ziweze kuwafikia Wananchi.