Watendaji wa Taasisi ya Wahasibu Wakaguzi na Washauri elekezi wa kodi Zanzibar ( ZIAAT ) wamesisitizwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao ili kuepuka malalamiko yanayoweza kuathiri utendaji wao wa kazi.
Akifungua Mkutano wa mwanzo kwa Watendaji hao Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Ndg. Ame Burhan Shadhil amesema lengo la Taasisi hiyo ni kusaidia kwa kiasi kikubwa kujadili njia bora ya kuimarisha utendaji wa kazi na kusimamia majukumu yao pamoja na kupima ubora wa huduma wanazozitoa na kukwepa makosa ya kikazi yanayoweza kujitokeza.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo Afisa Mwandamizi wa (ZIAAT ) Dk.Khamis Mohammed Khamis amesema fani ya uhasibu ni miongoni mwa fani zenye faida kwa maendeleo ya Nchi hivyo wafanye kazi kwa uadilifu ili kufikia lengo linalihitajika.
Washiriki wa Mkutano huo kutoka Aniste Consultant Ndg.Andrea Mabula na Ndg. Aziza Amour Abdallah kutoka Aniste Consultant wamesema Taasisi hiyo itasaidia kuipa hadhi fani ya uhasibu hasa katika kupata fursa za ajira kwa wenye taaluma hiyo.
Taasisi ya ZIAAT imeanzishwa Mwaka 2023 na ina jukumu la kuwasajili Wahasibu na kuwaongezea taaluma katika masuala yote ya kifedha ikiwemo kodi na ukaguzi