Waandishi wa Habari Kisiwani Pemba wametakiwa kutumia nafasi yao katika kuvitangaza vivutio vya utalii Kisiwani humo ikiwa na lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali kukifunguwa Kisiwa hicho Kitalii na kuimarisha uchumi wa Nchi.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea eneo la Kihistoria huko Chwaka Tumbe ikiwa ni ziara iliyoandaliwa na Wizara ya Utalii na mambo ya kale kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa habari Kisiwani Pemba .
Amesema ni vyema waandishi wa habari kuwapatia Wananchi Taarifa sahihi juu ya maendeleo makubwa yaliyopatikana Nchini,kupitia Sekta mbali mbali ikiwemo Sekta ya Utalii pamoja na kuunga Mkono juhudi hizo ili kuweza kupiga hatua zaidi za Kimaendeleo.
Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Utalii na mambo ya kale Zuhura Mgeni Othman amesema Sekta ya Utalii ni Sekta Mtambuka ambayo inachangia kwa kiasi Kikubwa Pato la Taifa hivyo ziara hiyo kwa Waandishi Wahabari kuvitangaza vifutio hivyo na kutowa Taaluma Wananchi waweze kuvitembelea kwa lengo la kujua Historia yao pamoja na kuchangia pato la Taifa ili malengo yaweze kufikiwa.
Nae Mwenyekiti wa Club ya Waandishi wa Habari Kisiwani Pemba Bakar Mussa Juma amesema Dhamira ya Club hiyo ni kuunga Mkono Utalii wa ndani na kuvitangaza Vivutio vya Utalii Kisiwani humo ili kuweza kukifunguwa Kiutalii na kuenuwa Uchumi.
Kisiwa cha Pemba kimebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii ambavyo Takribani vivutio 45 tayari vimekwisha kutambulika rasmi ikiwemo Mkamandume,Rasi mkumbuu ,Chakwa Tumbe na 15 bado vinaendelea kufanyiwa utafiti wa awali huku Mkoa wa Kaskazini Pemba ukitajwa kuongoza kwa maeneo mengi ya Kiutalii.