Wananchi wa Kata ya Mnali Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wameishukuru Serikali kwa kuanza Ujenzi wa Jengo la Wodi ya Wazazi katika Zahanati ya Kata hiyo.
Hatua ya Serikali kujenga Wodi hiyo imekuja baada ya kuwa na tatizo la ufinyu wa Chumba cha kujifungulia katika Zahanati hiyo hali iliyowalazimu Wananchi kujitolea kuanza kujenga Wodi ya Miti pembezoni mwa Zahanati hiyo Mwaka 2022.
Wakizungumza na ZBC Wananchi hao wamesema wanaipongeza Serikali kwa kuanza kuchukua hatua ya kujenga Jengo hilo ambapo kiu kubwa kwa sasa ni kuona Jengo hilo linakamilika na kuanza kutumika
Dokta Wilfred Makomba ni Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mnali anaeleza jinsi wodi hiyo itakavyorahisisha utendaji kazi na utoaji wa huduma pindi itakapokamilika.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Juma Mnwele amesema Ujenzi wa Wodi hiyo inajengwa kwa mapato ya ndani ambapo kwa awamu ya kwanza ulitengewa kiasi cha Shilingi Milioni 30 ambayo imefikisha jengo hilo katika hatua nzuri.