Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuanzishwa kwa Kituo cha pamoja cha Forodha baina ya Mataifa hayo ili kuongeza fursa za Biashara.
Hayo yameelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es salam wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa Ziara ya Siku Tatu ya Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi ambapo amesema bado mahusiano ya kibiashara baina ya Mataifa hayo yako chini.
Rais Samia ametaja Maeneo mengine ya ushirikiano waliyokubaliana ni pamoja na ulinzi na usalama, kilimo cha Zao la Korosho, Sekta ya Afya, Biashara na Uwekezaji.
Kwa upande wake Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi ameishukuru Tanzania kwa mchango wake wa ulinzi na usalama hasa katika Mipaka katika kukabiliana na changamaoto ya ugaidi.
Rais Nyusi yupo Nchini kwa Ziara ya Siku Tatu ambapo Kesho anatarajia kuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (SabaSaba) ambapo ataambatana na Mwenyeji wake Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.