Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali zote mbili za Tanzania zinatambua umuhimu na mchango mkubwa wa Wanawake katika hatua mbalimbali za maendeleo ikiwemo kumlinda na kumwezesha Kiuchumi.
Akifungua Kongamano la uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Zanzibar katika kusherehekea siku ya Wanawake Duniani kwa Niaba ya Dk Mwinyi huko Golden Tulip Uwanja wa Ndege Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema harakati hizo zinatokana na kutambua maendeleo yao ikiwemo ya Kiuchumi, Kijamii na kisiasa kwa lengo la kuhakikisha Mwanamke wanawezeshwa kushiriki katika fursa za Kimaendeleo.
Aidha ametoa wito kwa Wadau mbalimbali wa Maendeleo kushirikiana na Chemba ya Wanawake Wafanya Biashara Tanzania ili kuipa nguvu na kuwawezesha Wanawake wengi zaidi Nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma ametoa Shukrani kwa Serikali zote mbili kwa kusimamia harakati za Wanawake ili kuona Wanafikia malengo yao.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha kuendeleza Wanawake Tanzania Bi Mercy Sila na mwenyekiti wa chama cha kuendeleza wajasiriamali Zanzibar Bi Tatu Tandu wamesema lengo la Kongamano hilo ni kuwapa Wanawake Taarifa na Muongozo muhimu ili kustawi katika shughuli zao.
Wakati huo huo Mhe Hemed ametembelea Mabanda ya maonesho na kupata maelezo ya Wajasiriamali na kutoa tunzo kwa Wajasiriamali bora.