Kamati ya kudumu ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi imeishauri ofisi za Makamu wa pili ya Rais kupitia Kamisheni ya kukabiliana na Maafa kuaandaa utaratibu wa kuupatia fedha Mfuko wa kukabiliana na Maafa ili yanapotokea maafa Serikali iwe na uwezo wa kuwasaidia Wananchi wake kupitia Mfuko huo.
Ushauri huo umetolewa na Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Chini ya Mwenyekiti wake Mh.Maryam Thain Juma mara baada ya kupokea Taarifa ya utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha robo ya pili Oktoba –Disemba kwa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais huko katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Tibirizi.
Pia kamati hiyo imeishukuru Ofisi ya Makamo wa Pili ya Raisi kwa Mashirikiano wanayoyaonyesha kwa Wafanya kazi na Viongozi pamoja na usimamiaji mzuri wa Miradi mbali mbali ikiwemo Miradi ya TASSAF.
Akisoma Taarifa ,Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Salhina Mwita Ameir amesema Ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo ya kuimarisha hali za kiuchumi za Walengwa wa Tassaf kupitia Mpango wa kunusuru Kaya Masikini na kuongezeka kwa fursa za ajira kwa Walengwa waliyopatiwa fedha za ruzuku ya uzalishaji.