Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah amesema kuimarika kwa biashara katika eneo la Afrika kutasaidia kupatikana fursa zaidi na bara hilo kuweza kujitegemea kiuchumi.
Akifungua mkutano wa 3 wa Mawaziri na mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa Eneo huru la Biashara Afrika (afcfta) huko katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi, amesema hatua hiyo itakuza nguvu na dhamira ya viongozi na waasisi wa nchi zao katika kujenga nguvu ya pamoja na kukuza uchumi.
Amesema pamoja na vikwazo vilivyo ndani ya Bara hilo ikiwemo kutokuwa na usalama wa kutosha na mawasiliano ya lugha lakini ni vyema kuutumia mkutano huo kwa kujadili mbinu bora za kubadilisha uchumi kwa kukuza elimu ya kibiashara na masoko.
Naye, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban amesema mkutano huo ni muhimu kwa bara la Afrika kutokana na kujadili masuala muhimu ya kibiashara ambapo pamoja na vikwazo vilivyopo ikiwemo miundombinu ya usafirishaji na uzalishaji duni umeonesha mafanikio ya kukuza biashara.
Aidha, amesisitiza kuwa katika mkutano huo kuwa eneo huru la biashara barani afrika ni msingi imara wa maendeleo ya bara letu la kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni AFCFTA itawezesha kujitegemea na kuwa na maamuzi na sauti ya pamoja yenye nguvu.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji Mhe. Shariff Ali Shariff amesema mkutano huo wenye lengo la kuijenga Afrika imara kiuchumi kwani wajenzi wa Afrika ni waafrika wenyewe hivyo waongeze kuwajibika kwa kuzalisha zaidi kupitia raslimali walizonazo.
Mwakilishi wa taasisi ya AFCFTA Dkt. Samir Hamrouni amesema mkutano huo ni muhimu katika kujadili mustakbali wa soko la afrika hasa katika kutumia masoko mapya ya ukanda huo kwa biashara za gari na nyenginezo.
Miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Kenya, Tunisia, Togo, Congo na wenyeji Tanzania ikiwemo Zanzibar.