Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani Pemba kuhakikisha ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja wamenunua Mtambo mpya wa kuchomea Takataka za Hospitali ili kuepusha madhara.
Akikagua uendeshaji na utoaji wa huduma katika Hospitali hiyo amesema Uongozi unatakiwa kujipanga kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana kwa wakati unaostahiki amesema kuwepo kwa Mtambo huo kutawasaidia Wafanyakazi kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Wakati huo huo Makamu wa Pili amekagua Mradi wa Skuli za Msingi Chanjaani Jombwe na Skuli ya Sekondari Ole zinazojengwa na mkandarasi Kampuni ya Mwinyi Building contraction na bench Mark & Engineering LTD amesema Serikali imeamua kuwekeza katika Sekta ya Elimu kwa kuhakikisha inaweka miundombinu bora ya elimu ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri. Naibu waziri wa elimu na mafunzo ya Amali mhe. Ali Abdulgulam Hussein amesema malengo ya Serikali kupitia wizara ya Elimu ni kuhakikisha inakamilisha miradi yote inayojengwa, kuongeza idadi ya Madarasa na Dahalia za kisasa ili Wanafunzi wote waingie Mkondo mmoja wa masomo.
Wakandarasi wanaojenga Miradi hiyo wamesema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha Ujenzi ambapo wanatarajia kuikabidhi Serikali hivi karibuni.
Miradi mengine iliyotembelewa na kukaguliwa ni Ujenzi wa Barabara ya Ukutini Mtangani, Ujenzi wa Soko la Samaki na Mboga Mboga Vitongoji na Ujenzi wa Kituo cha Kuchomea takataka Vitongoji.